Menu
Close

Ludovick S.L. Utouh

Bwana Ludovick S.L. Utouh amezaliwa Tarehe 19 Septemba 1949 katika Kijiji cha Shidere, Tarafa ya Mkuu, Wilaya ya Rombo, Mkoa wa Kilimajaro.Ana mke mmoja Bi. Dr. Justina Lily Utouh. Mungu amembariki kupata watoto wanne; Magdalena Malaswai Utouh, Geofrey Lemnge Utouh, Michael Mrinde Utouh na Lucas Manshubi Utouh. Pamoja na wajukuu; Lucas Manshubi Utouh, Daniela Damas Kinemo, Alexandria Godfrey Utouh, Ludovic Mrinde Utouh, Lois Lucas Utouh, Gracious Damas Kinemo, Louis David Marealle, Lucresia Mrinde Utouh naTumaini Grace Lucas Utouh.

  1. Elimu Yake
  1. Shule ya Msingi/kati

Bwana. Ludovick S.L. Utouh alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi Mharu iliyopo katika Kijiji cha Shidere, Tarafa ya Mkuu, Wilayani Rombo, Mkoa wa Kilimanjaro kuanzia mwaka 1961. Aliendelea na masomo ya kati (middle school) kuanzia mwaka 1964 katika shule ya Kiomboi Shule ya Msingi iliyopo Kiomboi, Singida.

  1. Shule ya Sekondari

Bwana Ludovick S.L. Utouh alisoma Shule ya Sekondari ya Bihawana na baadae kujiunga na Shule ya Sekondari ya Shinyanga (Shinyanga High) mpaka mwaka 1969, alipohitimu masomo yake ya Sekondari. Kama ilivyokuwa ada katika kipindi hicho baada ya kuhitimu elimu ya sekondari alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa mnamo mwaka 1970 Makutopora (Operation Vitendo)

  • Elimu ya juu

Bwana Ludovick S.L. Utouh alijiunga na Taasisi ya Maendeleo na Utawala (IDM) Mzumbe na kuhitmu mwaka 1975. Baada ya hapo alijiunga na Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Algonquine kilichopo Ottawa, nchini Canada kuanzia mwaka 1978 mpaka 1981. Kisha alijiendeleza pia nchini Uingereza katika Chuo Kikuu cha Birmgham mpaka mwaka 1983 na mwaka 1995 alijiendeleza katika taasisi ya Mananga iliyopo Swaziland.

 

  1. Sehumu alizofanya Kazi

Bwana Ludovick S.L. Utouh alishafanya kazi katika taasisi mbalimbali akiwa ameshika nyadhifa mbali mbali kulingana na taaluma yake kama ifuatavyo;

  • 1969 –Mhasibu, Mara Cooperative Union
  • 1970 – Mhasibu, National Textile Company (NATEX)
  • 1975 -1976 Mhasibu, Taasisi ya Maendeleo na Utawala (IDM) Mzumbe
  • 1977 – Mwelekezi Msaidizi, Taasisi ya Maendeleo na Utawala (IDM) Mzumbe
  • 1980 – Mhadhili Msaidizi, Taasisi ya Maendeleo na Utawala (IDM) Mzumbe
  • 1983 – Mhadhiri, Taasisi ya Maendeleo na Utawala (IDM) Mzumbe
  • 1986 – Mhadhiri Mkuu, Taasisi ya Maendeleo na Utawala (IDM) Mzumbe
  • 1987 – Msajiri, Bodi ya Taifa ya Wahasibu (Registrar  – National Board of Accountants and Auditors NBAA)
  • 1995 – Mkurugenzi Mtendaji, Bodi ya Taifa ya Wahasibu (Executive Director – National Board of Accountants and Auditors NBAA)
  • 2006 mpaka 2014 – Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali (Controller and Auditor General (CAG))
  • 2015 – Executive Director and founder, Institute of Public Accountability

 

Bwana Ludovick S.L. Utouh pia anashika na amewahi kushika nyadhifa katika Taasisi za Elimu, Umma na Binafsi tofauti tofauti kama;

  • Kilimanjaro Hotel. (Mwenyekiti wa bodi)
  • AFROSAI – E (Mwenyekiti wa Bodi)
  • Taasisi ya Maendeleo na Utawala Mzumbe (IDM Mzumbe)
  • Chuo Kikuu cha Mzumbe( Mzumbe University)
  • Chuo cha Utawala wa Fedha (Institute of Financial Management,IFM)
  • Chuo cha Biashara (College of Business Education, CBE)
  • Chuo cha Wahasibu Tanzania (Tanzania Institute of Accounts)
  • Chuo cha Wahasibu Arusha (Institute of Accountancy of Arusha)
  • Duka la Hisa la Dar es Salaam (Dar es Salaam Stock Exchange)
  • Umoja wa Kimataifa wa Wahasibu (International Federation of Accountants (IFAC),

 

 

 

 

2.0: Ufanisi katika Kuleta Uwajibikaji na Udhibiti Wa Matumizi Mabaya ya Rasilimali za Umma

 

Bw. Ludovick S.L. Utouh, alistaafu rasmi kwa heshima kubwa, kutoka kwenye nafasi ya Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali Tarehe 19 Septemba 2014, baada ya kuitumikia nafasi hiyo kwa miaka saba na miezi kumi tangu alipoteuliwa Tarehe 19 Agosti, 2006. Ameacha historia kwa kutekeleza kazi na wajibu wake kama Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 143 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 (iliyorekebishwa 2005) kama ilivyofafanuliwa zaidi na vifungu vya 45 na 48 vya sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Na. 9 ya Mwaka 1982 (ilivyorekebishwa 2000) na kifungu Na.10 (1) cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma ya Mwaka 2008.

Bw. Ludovick S.L. Utouh katika uongozi wake alisimamia na kutekeleza vema Dira ya Ofisi ya Mkaguzi Mkuu inayosema kuwa Ofisi hiyo ni Kituo cha ubora katika ukaguzi wa hesabu katika sekta za umma. Lengo la Ofisi ni Kutoa huduma bora za ukaguzi zenye kuleta tija kwa nia ya kuimarisha uwajibikaji na thamani ya fedha katika kukusanya na kutumia rasilimaliza umma.

Katika utekelezaji wa kazi na wajibu wake wa Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serekali Bw. Ludovick S.L. Utouh alifanya na kuongoza mambo mengi, yenye lengo la Kuboresha, Kutetea, Kulinda na Kuendeleza misingi ya Utawala Bora. Hili lilionekana katika kuboresha usimamizi wa rasilimali za nchi kama ifuatavyo;

2.1:      Ushawishi wa kuanzishwa kwa Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani (Internal Auditor General);

Kwa kutambua umuhimu wa ukaguzi wa ndani, alisisitiza kuanzishwa kwa Idara ya Mkaguzi wa Ndani wa Serikali (Internal Auditor General Division) ambayo ina jukumu la kusimamia na kuboresha ukaguzi wa ndani kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa na Sekrietarieti za Mikoa. Hili linilenga kuongeza wigo na kupunguza mianya ya rushwa, upotevu wa pesa na misharaha hewa. Ambapo wakaguzi wa ndani wa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa wanahakikisha hesabu za miradi yote ya maendeleo katika maeneo yao ya kazi zinakaguliwa ili kuhakikisha kuwa inatoa matokeo mazuri yanayolingana na thamani ya fedha kwa matumizi yaliyofanywa.

2.2:      Ushawishi kuondolewa kwa Wabunge katika Bodi za Mashirika ya Umma

Bw. Ludovick S.L. Utouh katika nafasi yake alikuwa akitoa mawazo ambayo yanajenga na kuzingatia Haki za Binadamu na Utawala bora. Alipendekeza kuwa wabunge na madiwani wasiteuliwe katika Bodi za Mashirika ya Umma kwani kuwepo kwao katika Bodi hizo kunasababisha mgongano wa kimaslahi. Bw. Utouh alisema kuendelea kwa wabunge kuzitumikia bodi za Wakurugenzi za Mashirika ya Umma na Taasisi nyinginezo kunatia dosari utendaji kazi za Bodi za Wakurugenzi. “Mwenendo huu ni kinyume na taratibu nzuri na ni kinyume na kanuni za utawala bora… wenzetu wanatucheka katika hili” Alisema wakati umefika kwa serikali kutoa waraka ambao utazuia wabunge kuwa wajumbe wa Bodi za Wakurugenzi za Mashirika ya Umma ili waweze kuhoji vyema mwenendo wa mashirika hayo.

2.3:      Mapendekezo ya kuboresha Sheria na miongozo mbalimbali na Uanzishwaji wa Sheria ya Ukaguzi wa Umma:

Bw. Ludovick S.L. Utouh na ofisi yake ilishawishi Serikali/Bunge kutunga Sheria ya Ukaguzi wa Umma na Mwaka 2008 Sheria hiyo ilitungwa pamoja na kanuni zake mwaka 2009. Sheria hii iliongeza wigo na uhuru wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika kutekeleza majukumu yake Kikatiba.

2.4:      Kuongezeka kwa Uwazi wa Taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serekali

Bw. Ludovick Utouh, aliimarisha na kuboresha Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ya Tanzania kimuundo, kiutendaji na kimaslahi na kuifanya taasisi hiyo ya serikali kwa mara ya kwanza kuwa huru, wazi na iliyoweka utaratibu mpya ambao hata mwananchi wa kawaida aliona kuwa wanayo haki ya kufuatilia na kujua hesabu za serikali yao ambayo inafanya matumizi kutokana na kodi yao. Hili linajidhihirisha bayana kwa kuangalia historia ya ofisi hii kabla ya miaka (7) saba iliyopita ambapo ofisi hii ilikuwa inadhaniwa kana kwamba haiwahusu wananchi wa kawaida.

Pamoja na hayo ofisi hiyo ilifanya kazi kwa ufanisi na kutoa taarifa za ukaguzi wa mahesabu kwa wakati kwa mujibu wa Sheria jambo lililowezesha taarifa hizo kuwa na tija na kuwawezesha wadau mbali mbali kuweza kuzitumia. Taarifa za ukaguzi ziliweza kuwafikia wananchi wa kawaida na wadau wengi kwa wakati na kwa lugha rahisi (Ikiwemo taarifa ya vikaragosi ambayo mtu yoyote aliweza kuielewa),na kwa kupitia tovuti ya ofisi hiyo.

2.5:      Kujenga na Kuboresha mahusiano mazuri kati ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bunge na Serikali.

Bw. Ludovick Utouh,katika uongozi wake alijenga na kuboresha mahusiano ya ofisi ya mkaguzi wa hesabu za serekali na mhimili wa Bunge na Serekali jambo ambalo lilileta tija kwa kazi ya ofisi kuonekana, taarifa zake kujadiliwa na wananchi na viongozi kudai kuheshimiwa na utekelezaji wa mapendekezo ya ripoti za Ukaguzi kwenye Serekali na Taasisi za Umma.

Mahusiano hayo pia yalipelekea ubadilishwaji wa kanuni za Bunge na kuwezesha ripoti za mkaguzi wa hesabu za serekali kujadiliwa moja kwa moja Bungeni kwenye vikao vya wazi. Hii iliwezesha umma wa watanzania kuelewa juu ya ripoti hizo na kukuza wingo wa ushiriki wa wadau wengi katika kudai uwajibikaji wa serekali na matumizi bora ya rasilimali.

Pia ushauri wake kwa mamlaka mbalimbali ulipelekea Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika vikao elekezi, kwa nyakati tofauti na Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Mamlaka za Serikali za Mitaa kusisitiza umuhimu wa kuzipitia na kuzifanyia kazi taarifa zinazotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Hii ilileta mwamko mpya katika kuona umuhimu wa ripoti hizi na kutumika kwake katika kufanya maamuzi mbalimbali serikalini.

Katika kuhakikisha mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali yanafanyiwa kazi, Serikali, chini ya Katibu Mkuu Kiongozi, iliunda Kamati ya Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Mapendekezo yanayotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika ripoti zake. Kamati hii ni ya kudumu inajukumu la kuhakikisha kwamba mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali yanafanyiwa kazi kwa wakati, na taarifa kutolewa.

2.5.1:   Kuongezeka kwa Bajeti ya Ofisi ya Ukaguzi:

Serikali iliboresha utaratibu na mchakato mzima wa kupitisha bajeti ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali uliowezesha bajeti ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kuongezeka kwa asilimia 306% katika kipindi cha miaka mitano, kuanzia mwaka wa fedha wa 2008/9 hadi 2013/14. Hii imetokana na mchango wa ofisi hiyo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wakati wa uongozi wake. Hiyo kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi. Ujenzi na ukarabati wa majengo ya ofisi hizo mbali mbali. Kuanzia mwaka 2008 Serikali iliongeza na kutoa vibali vya kuajiri watumishi wa kada mbalimbali kwa kuzingatia mahitaji ya ofis. Kwa lengo la kuimarisha ofisi hii kiutendaji. Pia, kuongeza watumishi wa Ofisi kupatiwa mafunzo mbalimbali ndani na nje ya nchi kupitia fedha za Serikali na za wafadhili mbalimbali

2.5.2:   Kushawishi kutumika kwa viwango vinavyokubalika kimataifa (IPSAS) vya uandaaji wa taarifa za fedha na Kuridhiwa kwa Mikataba ya Kimataifa:

Hali kadhalika, chini ya Uongozi wake ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, imejenga mahusiano na  Ofisi za Wadhibiti na Wakaguzi Wakuu wa Hesabu za Serikali za nchi mbalimbali. Serikali iliridhia Azimio la Umoja wa Mataifa Na. A/66/209 linalohusu kuwepo kwa ufanisi, uwajibikaji, tija na uwazi katika usimamiaji wa rasilimali za umma kwa kuimarisha Ofisi za Taifa za Ukaguzi Tarehe 22 Desemba 2011. Hii imesaidia sana Ofisi kutambulika na kukubalika kimataifa. Kuipa sifa na Kuiwezesha Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kuwa mshiriki katika Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa. Pia kuwezesha Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kupata tuzo ya Taasisi bora za Ukaguzi barani Afrika kwa nchi zinazoongea Kiingereza “AFROSAI-E award”. Kujulikana kwa Ofisi kitaifa na kimataifa ambapo imeweza kupata kazi za kimataifa na kuwa mwanachama katika taasisi mbalimbali za kimataifa kama vile AFROSAI-E ,INTOSAI na nyinginezo.

 

3.0:      Kutambuliwa kwa Mchango wake na Kitaifa na Kimataifa

Bwana Ludovick Utouh ametoa mchango wake mkubwa kwenye nyadhifa ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serekali . Mchango huu umetambuliwa na wadau mbalimbali kama;

  1. Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, alimtunuku Nishani ya Utumishi Mrefu na Maadili Mema mnamo Tarehe 9 Desemba 2012.
  2. Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serekali iliimpa tuzo ya Utendaji Uliotukuka
  • Umoja wa Mataifa (UNGA) uliichagua Tanzania kuwa Mjumbe wa Bodi ya Ukaguzi ya Umoja huo, kwa kipindi cha miaka sita kuanzia Julai 1, 2012 mpaka Juni 2018, wakati wa uongozi wake.
  1. 2015 Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kina mtunuku “Maji Maji Human Right Award” kwa kutambua mchango wake wa kulinda na kutetea haki za binadamu kwa kusimamia kuheshimuji wa misingi ya Utawala Bora na Utawala wa Sheria.

 

 

 

 

4.0:      Sababu za kumpa Tuzo za Majimaji za Haki za Binadamu                              

 

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ni shirika lisilo la serekali lenye kujibidisha katika kulinda, kutetea  na kuendeleza Haki za Binadamu na Utawa Bora nchi. Kituo hufanya hivi kupitia utekelezaji wa program zake mbali mbali  ikiwemo ufuatiliaji wa utendaji wa Bunge na Utendaji wa Serekali. Ndio maana katika kazi zake zimeona mchango wa Ndugu Ludovick Utouh.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu katika kufanya kazi yake ya uangalizi wa Bunge huhudhuria mijadala ya Bunge Dodoma, hupitia kumbukumbu za majadiliano ya bunge (hanzards), hurekodi majadiliano ya Bunge kama yanavyorushwa moja kwa moja kwenye vipindi vya luninga. Kutokana na majadiliano ya Bunge  na uchambuzi uliofanywa na Kituo imeonekana dhahiri mchango wa Bwana Utoh katika kusaidia kukuza uwazi na usimamizi bora wa rasilimali za umma kupitia ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti wa hesabu za serekali. Pia katika kipindi chale aliongoza uchunguzi wa ziada wa matumizi mabaya, ubadhilifu na ufujwaji wa rasilimali za umma mathalani ;

  • 2006 – Ripoti za Ukaguzi ilionyesha ugawaji wa zabuni ya kutengeneza Umeme wa dharura kwa kampuni hewa ya Richmond/ Dowans Electricity wa Tsh 172 Billioni na Utoaji wa tuzo la Dolla 137,000 kwa siku katika kutoa mega watts 100 za umeme ambao haukutolewa japo fedha hizo zililipwa.
  • Ufisadi wa mabilioni ya shilingi kupitia ununuzi wa rada kuu kuu kutoka Kampuni ya Uingereza British Aerospace Engineering (BAE Systems). Ununuzi wa rada hiyo ulitajwa kutofuata taratibu sahihi, uliligharimu taifa TSh 70 bilioni, wakati gharama halisi ilikuwa TSh 21 bilioni.
  • 2008 – Ripoti za ukaguzi ziliweka wazi utoaji wa fedha uliofanywa kiholewa kutoka kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (External Payment of Arreas – EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Fedha hizi za Tshillings 133 Billioni zilinukuliwa kugawiwa kiholela kwa makampuni 22.
  • 2014 – Ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu liliweka wazi matumizi holela ya fedha kutoka kwenye akaunti ya Tegeta ESCROW katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Akaunti hiyo iliyokuwa na zaidi ya Tsh200 bilioni. Akounti hii ilifunguliwa wakati kukiwa kuna mgogoro wa kisheria baini ya wabia wa zamani wa IPTL (VIP Engeneering and Marketing na Mechmar Corporation ya Malaysia) kwa upande mmoja, Tanesco na Independent Power Tanzania, IPT, kwa upande mwingine.

Hii ni baadhi tuu ya mifano ya ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serekali chini ya Uongozi wa Bwana Utouh zilizoonyesha umakini na misingi aliyonayo ya kuhakikisha uheshimuji wa misingi ya utawala bora na  utawala wa sheria. Ripoti hizi zimefungua wigo wa majadiliano ya kitaifa juu ya usimamizi wa rasilimali, wajibu wa viongozi na raia katika kuhakikisha kuwa rasilimaji za nchi zinawanufaisha wananchi wote na kudai uwajibikaji wa viongozi.

Misingi hii imeonekana dhahiri katika majadiliano mbali mbali na hususani kwenye mchakato wa uandaaji wa Katiba mpya.

 

HITIMISHO

Kutokana na Umahiri wa Bwana Ludovick Utouh,  katika utendaji wake amewezesha kuimarika kwa baadhi za Taasisi za Serikali na za Umma katika eneo la utawala bora, maadili na udhibiti wa rasilimali za Taifa ikiwemo; Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi yenyewe, kuongezeka uhuru wa Ofisi hiyo, uwazi wa taarifa zake na kuboreshwa kwa sheria za Ukaguzi. Pia amesaidia wananchi kupata taarifa za ripoti za ukaguzi na kusaidia waweze kushiriki kuhoji na kudai uwajibikaji wa serekali kwa raia. Mchango wake huu ndio umefanya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kumtunuku Tuzo ya Maji Maji kwa Mwaka wa 2015.

Leave a Comment